BIN SLUM TYRES KUFUNGUA DIMBA KOMBE LA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN

MICHUANO maalum ya kuwania Kombe la mwezi mtukufu wa Ramadhani inatarajiwa kuanza Jumamosi wiki hii Uwanja wa JMK Centre, yaani Kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa zamani wa Tanzania, siku moja tu tu baada ya sherehe zake za ufunguzi Ijuma ya Mei 18
Michuano itafunguliwa kwa mchezo maalum wa maveterani Ijumaa kabla ya Jumamosi kufanyika mechi mbili za Kundi A kati ya Bin Slum Tyres & Risa FC dhidi ya Dar Athletics FC kuanzia Saa 4:00 usiku, kabla ya Simba Oil FC kumenyana na Somali FC kuanzia Saa 5:00 usiku.

Kundi B linaundwa na timu za Asas Rangers, Rajaa, State Oil na Scaba Scuba, wakati Kundi C linaundwa na Al Mahra, Usangu FC, Astra Line na Istiqama na Kundi D linaundwa na Al Maghaj, Bin Maksoor, Katalunya na Kariakoo Bazaar.
Michuano hiyo ambayo imekuwa ikifanyika tangu miaka ya 1990, kwa mara ya kwanza ilionyeshwa moja kwa moja na Azam TV mwaka jana na Skywards wakaibuka mabingwa wakiwafunga Balhaboub katika fainali.
Hata hivyo, msimu huu mabingwa hao watetezi hawajajitokeza kutokana na wachezaji wao wengi kuchukuliwa na Asas Dairies.